Sherehe za Waamasai za Kuwapa Majina Watoto

Sherehe za Kimaasai za Utoaji Majina kwa Watoto

Mtoto wa Kimaasai anapozaliwa, hapatiwi jina rasmi, ila hupewa jina la muda tu linajulikana kama embolet, ikiwa ina maana ya Ufunguzi. Toka siku alipozaliwa, mpaka siku itakapofanyika sherehe ya kumpatia jina, mtoto atakuwa akitambulishwa kwa kutumia jina la embolet. Watoto wa Kimaasai huwa wanatofautiana kiumri wakati sherehe ya kutoa majina inapofanyika. Kutegemea na koo za familia zao, baadhi yao wanaweza kuwa na umri unaofikia miaka mitatu kabla ya kufanyika kwa sherehe ya kutoa majina, ambayo hujulikana kama Enkipukonoto Eaji ikimaanisha kutoka katika kujifungia ndani/kujitenga. Katika kuelekea kwenye sherehe za Enkipukonoto Eaji, mama na mtoto uwa wanakaa ndani na kuruhusu nywele ziote na zirefuke.

Maasai wakichoma nyama
Maasai wakichoma nyama

Sherehe zinapoanza, uwa wanatoka ndani na vichwa vyao hunyolewa, kitendo ambacho ni cha kawaida katika sherehe nyingi za ibada za njia za Wamaasai. Maandalizi ya sherehe za kutoa majina huchukua mpaka siku mbili na huhusisha shughuli mbalimbali. Kwanza wadhamini wawili, ambapo mmoja uwa kwa ajili ya mama na mwingine kwa ajili ya mtoto, huchaguliwa wakati wa sherehe. Kila mfadhili haina budi kuwa katika kundi linalolingana na umri wa mama au mtoto na hubakia kuwa na uhusiano wa karibu sana na familia. Kisha kondoo dume wawili huchaguliwa, ambapo mmoja huchinjwa na kutumiwa kama kitoweo siku zote sherehe itakapokuwa ikiendelea.

Ni wanawake pekee wanaoruhusiwa kula nyama ya kondoo huyu. Hii hufanyika kwa ajili ya kuwafurahisha wanawake na kujaribu kulipia maumivu waliyohisi wakati wa kujifungua. Pia wanawake hula nyama kama njia ya kutoa shukurani kwa Engai, hili ni neno la Kimaasai linalomaanisha Mungu, au Kiumbe mkuu., kwa kuwapatia uwezo wa kuzaa watoto. Kisha mama huweka Olkererreti, ambayo ni bangili iliyotengenezwa  kwa kutumia mguu wa kulia wa kondoo, kwenye mkono wa kulia wa mtoto. Kisha kibuyu maalumu cha Kimaasai hutumika kuchota maji katika mto. Mama hunywa maji haya pale sherehe inapoanza.

Pale nyama inapokuwa tayari na shughuli zote tulizoziorodhesha hapo juu zikiwa zimekamilika, mama hupewa maji katika kibuyu ili ayanywe, na mfadhili wa mama hutangaza kuwa sherehe imeanza. Wanawake wengine hujumuika pamoja na mama na mfadhili wake, kisha huanza kutathimini embolet ya mtoto na kuamua jina lake jipya kutegemea na haiba ya mtoto toka alivyozaliwa. Ikiwa watu wengi wanapenda jina lake la muda mfupi, kuna uwezekano wa kuendelea kutumika. Wanawake humbariki mtoto na jina lake jipya kwa kusema “Jina hili liishi ndani yako” na hilo jina jipya linalojulikana kama enkama enchorio, huwa ni la kudumu. Mwisho, mama huondoa bangili ya mtoto na sherehe huisha.

Kwa kawaida Wamaasai huishi katika makazi ya kifamilia yaliyozungushiwa uzio ambayo hujulikana kama maboma na hujumuisha nyumba chache na ng’ombe. Wakati wa siku mbili za sherehe ya kutoa jina, mama wa mtoto pamoja na mtoto hupewa heshima ya kuwa ndiyo wenye mamlaka ya pekee ya kuweza kufungua na kufunga lango la boma.

Kwa nakala zaidi zinazohusu kabila la kimaasai bofya hapa!