Mwanamazingaombwe na Mwana wa Sultani
Orodha ya Yaliyomo
Hapo zamani kulikua na sultani aliyekuwa na watoto watatu wa kiume, ambao hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kuwafundisha chochote kile; hali ambayo iliwahuzunisha sana sultani na mkewe.
Siku moja mwanamazingaombwe alikuja kwa sultani na kusema, “Ikiwa nitawachukua watoto wako watatu wa kiume na kuwafundisha kusoma na kuandika, na kuwafanya wasomi wakubwa , utanipa nini?”
Sultani akasema, “Nitakupa nusu ya mali zangu.”
“Hapana,” alisema mwanamazingaombwe; “Hiyo haitafaa.”
“Nitakupa nusu ya miji ninayoimiliki.”
“Hapana; hiyo haitanitosha. ”
“Unataka nini, basi?”
“Nitakapowafanya wasomi na kuwarudisha kwako, chagua wawili kati yao na unipe wa tatu; kwasababu nataka kuwa na rafiki yangu wa karibu. ”
“Nimekubali,” alisema sultani.
Mwanamazingaombwe aliwachukua, na cha kushangaza aliwafundisha kusoma na kuandika barua na kuwafanya wasomi wazuri sana kwa muda mfupi. Kisha akawarudisha kwa sultani na kusema: “Hawa hapa watoto. Wote ni wasomi wazuri kwa usawa. Chagua. ”
Nyumbani kwa Mwanamazingaombwe
Sultani aliwachukua watoto wawili aliowapenda, na mwanamazingaombwe akaondoka na yule wa tatu, ambaye jina lake lilikuwa Keejaa’naa, kwenda kwenye nyumba yake, ambayo ilikuwa kubwa sana.
Walipofika, Mchaa’wee, ambaye ndie mwanamazingaombwe, alimpa kijana yule funguo zote, akisema, “Fungua chochote utakacho.” Kisha akamwambia kuwa yeye ndiye baba yake, na kuwa anasafiri kwa muda wa mwezi mmoja.
Udukuzi wa Keejaa’naa
Alipokuwa ameondoka, Keejaa’naa alichukua funguo na kwenda kuchunguza nyumba. Alifungua mlango mmoja na aliona chumba kimejaa maji ya dhahabu. Aliweka kidole chake ndani, na dhahabu iling’ang’ania kwenye kidole, alijaribu kuifuta na kuisugua awezavyo lakini dhahabu haikutoka; Alijifunga kipande cha kitambaaa, na wakati baba yake aliporudi nyumbani na kuona kile kitambaa, alimuuliza amekifanya nini kidole chake, aliogopa kumwambia ukweli, alisema kwamba alijikata.
Punde si punde baada ya Mchaawee kuondoka tena, kijana huyo alichukua funguo na kuendelea na uchunguzi wake.
Chumba cha kwanza alichofungua kilikuwa kimejaa mifupa ya mbuzi, cha pili kilikuwa na mifupa ya kondoo, cha tatu kilikuwa na mifupa ya ng’ombe, cha nne kilikuwa na mifupa ya punda, cha tano kilikuwa na mifupa ya farasi, cha sita kilikuwa na mafuvu ya binadamu na cha saba kulikuwa na farasi aliokua hai.
Farasi wa maajabu na mpango wa kutoroka
“Habari!” alisema farasi; “Unatokea wapi, wewe ni mwana wa Adamu?”
“Hii ni nyumba ya baba yangu,” alisema Keejaa’naa.
“Ah, kweli!” lilikuwa jibu. “Sawa, una mzazi mzuri sana! Je! Unajua kwamba anajihusisha na kula watu, punda, farasi, ng’ombe, mbuzi na kila kitu anachoweza kuweka mikononi mwake? Mimi na wewe ndio viumbe hai tuliobakia. ”
Hii ililimuogopesha sana kijana yule, na alianza kubabaika, “Tufanye nini?”
“Jina lako nani?” Aliuliza farasi.
“Keejaa’naa.”
“Jina langu ni Faaraa′see. Sasa, Keejaa’naa, kwanza kabisa, njoo unifungnue. ”
Kijana yule alifanya hivyo mara moja.
“Sasa, basi, fungua mlango wa chumba chenye dhahabu ndani yake, nami nitameza yote; halafu nitakwenda kukusubiri chini ya mti mkubwa ulioko barabarani kidogo. Wakati mwanamazingaombwe atakaporudi nyumbani, atakuambia, “Twende tukatafute kuni;” kisha utajibu, ‘Sielewi jinsi ya kufanya kazi hiyo ;’ na atakwenda peke yake. Atakaporudi, ataweka chungu kikubwa sana kwenye jiko na atakuambia uwashe moto chini ya chungu hicho. Utamwambia hujui jinsi ya kuwasha moto, naye atauwasha mwenyewe.
“Halafu ataleta siagi nyingi, na inapoendelea kuchemka ataweka bembea na atakuambia, ‘Njoo nitakusukuma ubembee.’ Lakini utamwambia haujawahi kucheza mchezo huo , na umwombe yeye abembee kwanza, ili uone jinsi unavyochezwa. Atainuka kukuonyesha; na lazima umsukume ndani ya chungu hicho kikubwa, kisha uje kwangu haraka iwezekanavyo. ”
Kisha farasi akaenda zake.
Mauaji ya mwanamazingaombwe
Mchaa’wee aliwaalika baadhi ya marafiki zake kwenye sherehe nyumbani kwake jioni hiyo; kwa hiyo, alirudi nyumbani mapema, akamwambia Keejaa’naa, “Twende tukatafute kuni;” lakini yule kijana alijibu, “Sielewi jinsi ya kufanya kazi hiyo.” Akaenda peke yake na akaleta kuni.
Kisha akaweka chungu hicho kikubwa na kusema, “Washa moto;” lakini yule kijana akasema, “Sijui jinsi ya kuwasha moto.” Mwanamazingaombwe aliweka kuni chini ya chungu na akawasha mwenyewe.
Kisha akasema, “Weka siagi yote kwenye chungu;” lakini yule kijana akajibu, “Siwezi kuinyanyua; Sina nguvu za kutosha. ” Mwanamazingaombwe aliweka siagi mwenyewe.
Baadae Mchaa’wee aliuliza, “Umewahi kuona mchezo wa nchini kwetu?” Keejaa’naa akajibu, “Sidhani kama nimewahi kuona.”
“Sawa,” alisema mwanamazingaombwe, “Tucheze wakati siagi inaendelea kuchemka.”
Alifunga bembea na akamwambia Keejaa’naa, “Njoo ujifunze huu mchezo.” Lakini yule kijana akasema: “Wewe nenda kwanza unionyeshe. Nitajifunza haraka zaidi kwa njia hiyo. ”
Mwanamazingaombwe alikaa kwenye bembea, na alipoanza tu kubembea Keejaanaa alimsukuma mpaka ndani ya chungu hicho kikubwa; na kwa wakati huo siagi ilikuwa ikichemka, haikumuua tu, bali ilimpika pia.
Mara tu baada ya kijana yule kumsukuma mwanamazingaombwe ndani ya chungu hicho kikubwa, alikimbia haraka iwezekanavyo kwenye mti mkubwa, ambapo farasi alikuwa akimsubiri.
“Njoo haraka” alisema Faaraa’see; “Panda mgongoni kwangu tuondoke.”
Akapanda na wakaanza kuondoka.
Wageni wa mwanamazingaombwe walipofika walimtafuta kila mahali, lakini hawakumpata. Baada ya kumsubiri kwa muda mrefu, walianza kupatwa na njaa kali; wakaanza kutafuta chakula, wakaona kitoweo kwenye chungu kikubwa kipo tayari,wakaanza kuambiana, “Tuanze kula” wakaanza kula kilichokuwemo ndani ya chungu. Baada ya kumaliza, walimtafuta Mchaa’wee tena, walikuta mahitaji ya kutosha ndani ya nyumba hiyo, walidhani watakaa hapo mpaka atakaporudi; lakini baada ya kusubiri kwa siku kadhaa na kula chakula chote mahali pale, walikata tamaa wakarudi majumbani kwao.
Maisha mapya ya Keejaa’naa
Wakati huo Keejaa’naa na farasi waliendelea na safari yao mpaka walipofika umbali mrefu sana, na mwishowe walisimama karibu na mji mkubwa.
“Tukae hapa,” alisema kijana, “na tujenge nyumba.”
Faaraa’see alikubali na wakafanya hivyo. Farasi aliikohoa dhahabu yote aliokuwa ameimeza, ambapo walinunua vijakazi, ng’ombe, na kila kitu walicho kihitaji.
Watu wa mji huo walipoona nyumba nzuri mpya na vijakazi wote, ng’ombe na utajiri uliomo, walienda kumwambia sultani wao, ambaye mara moja aliamua kuwa mmiliki wa eneo kama hilo atakuwa ana umuhimu mkubwa wa kutembelewa na kutambuliwa kama mtu wa muhimu katika jamii.
Alimwita Keejaa’naa, na kumuuliza yeye ni nani.
“Ah, mimi ni mtu wa kawaida tu, kama watu wengine.”
“Wewe ni msafiri?”
“Nilikuwa; lakini napenda mahali hapa, na nadhani nitakaa hapa. ”
“Kwa nini usije kutembelea mji wetu?”
“Ningependa sana, lakini ninahitaji mtu wa kunitembeza.”
“Ah, nitakutembeza karibu,” sultani alisema, kwa shauku, kwani alishawishika sana na yule kijana.
Baada ya maongezi hayo Keejaanaa na sultani wakaishia kuwa marafiki wakubwa; na baada ya kipindi kirefu kupita kijana huyo alioa binti ya sultani, na wakajaaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume pamoja.
Waliishi pamoja kwa furaha sana, na Keejaanaa alimpenda Faaraasee kama roho yake mwenyewe.
Kwa nakala zaidi zinazohusu hadithi bofya hapa!