Kijana mwindaji - Mkaa Jikoni

Mkaaah Jeechonee (Mkaa Jikoni), Kijana Mwindaji 

Orodha ya Yaliyomo

Sehemu ya Kwanza

Sultani Maaj′noon alikuwa na watoto saba, na paka mkubwa, vitu ambavyo vilimfanya ajionee fahari sana.

Kila kitu kilienda vizuri, hadi siku moja paka alipomkamata ndama. Walipomfikishia taarifa sultani akasema, “Jambo jema, paka ni wangu, na ndama ni wangu.” Hivyo wakamjibu “sawa, mkuu,” basi tuliache suala hili.

Siku chache baadae yule paka alimkamata mbuzi; na walipomwambia sultani akasema, “paka ni wangu, na mbuzi ni wangu;” kwahiyo suala hilo likaisha tena.

Baada ya siku mbili tena, yule paka alimkamata ng’ombe. Walipomwambia sultani, aliwafunga midomo kwa kuwaambia, “paka wangu, na ng’ombe wangu.”

Baada ya siku mbili paka alimkamata punda; matokeo yakawa yaleyale.

Baadae alimkamata farasi; matokeo yakawa yaleyale.

Aliyefuatia kukamatwa alikuwa ni ngamia; na walipomwambia sultani alisema “mna tatizo gani nyie watu? Alikuwa ni paka wangu, na ngamia wangu. Naamini hammpendi paka wangu, na mnataka auliwe, mnaniletea hadithi hizi kila siku. Muacheni ale chochote anachotaka.”

Ndani ya mda mfupi alimkamata mtoto, kisha akamkamata mwanaume mtu mzima; ila kila wakati sultani alikuwa akisema kuwa paka na waathirika wote ni mali yake, na hakufikiria zaidi ya hapo.

Baada ya muda paka alianza kuwa jasiri, akawa anatembelea sehemu zilizo karibu ya mji, akiwabwekea na kuwala watu wanaoenda kuchota maji, au wanyama walioko malishoni.

Hatimaye baadhi ya watu walipata ujasiri, wakaenda kwa sultani, wakamwambia “hili suala likoje, mkuu? Kwakuwa wewe ni sultani basi ni mlinzi wetu,─ au unapaswa kuwa mlinzi wetu,­─ na sasa umeamua kumuacha huyu paka afanye atakavyo, na kwasasa anaishi nje ya mji, na anaua kila kiumbe hai kinachomkaribia, na wakati wa usiku anakuja mjini na kufanya kitu kilekile. Sasa, tutafanya nini katika hii dunia?”

Ila Maajnoon aliwajibu akisema :  “Ninaamini mnamchukia paka wangu. Na mnataka nimuuue; ila sitafanya hivyo. Kila kitu anachokula ni cha kwangu.”

Watu wote walishangazwa na matokeo ya ule usaili, na hakuna hata mmoja aliyethubutu kumuua paka, wote waliamua kuhama maeneo jirani na paka alipokuwa anaishi. Ila bado hali haikutulia, baada ya paka kutowaona watu wakipita, aliamua kuhamisha makazi yake pia.

Watu walizidi kulalamika, mpaka mwisho wake Sultani Maajnoon aliamuru kuwa mtu atakayeleta mashtaka juu ya paka, asiruhusiwe kuonana naye.

Baada ya watu kuamua kujifungia majumbani pamoja na mifugo yao, paka aliamua kuingia ndani ya mji, akaua na kula ng’ombe, ndege, na kila alichokuwa anakutana nacho.

Siku moja sultani aliwaambia wanae wa kiume sita, “ninaenda kuungalia mji leo; twendeni wote.”

Mtoto wa saba alionekana ni mdogo asiyeweza kwenda popote, na siku zote walikuwa wanamuacha na wanawake nyumbani, kaka zake walikuwa wanamwita Mkaa′ah Jeecho′nee, ikimaanisha Bwana mkaa jikoni.

Baada ya kutembea kwa mda walifikia kichaka. Baba alikuwa mbele, na watoto wakimfuata, mara ghafla paka aliwarukia na kuwaua watoto watatu kutoka mwisho.

Watumishi wa mfalme walipiga kelele, “paka! paka!” na wanajeshi waliomba ruhusa ya kumtafuta na kumuua, sultani alitoa ruhusa hiyo bila kusita akisema:“huyu siyo paka, ni noon’dah. Amewachukua wanangu.”

Kwasasa, hakuna mtu aliyewahi kumuona noondah, ila kila mmoja alijua kuwa ni mnyama hatari anayeweza kuua na kula viumbe wengine.

Wakati sultani alipoanza kuomboleza vifo vya wanae, baadhi ya watu waliomsikia walimwambia: “mkuu, huyu noondah hachagui wa kumla. Hawezi kusema: ‘Huyu ni mtoto wa mkuu, nitamuacha,’ au, ‘Huyu ni mke wa mkuu, sitamla.’Tulipokwambia alichofanya paka, siku zote ulisema alikuwa ni paka wako, na alichokula ni chako, na sasa amewaua watoto wako, na hatuamini kama anaweza sita kukula hata wewe.”

Na alisema, “Ninahofia mnasema ukweli.”

Wanajeshi waliojaribu kumkamata paka, baadhi waliuliwa na wengine walikimbia, na sultani na wanae waliobaki walichukua miili ya marehemu na kwenda kuizika nyumbani.

Baada ya Mkaa Jikoni, aliyekuwa mtoto wa saba, kusikia kuwa kaka zake wameuliwa na noondah, alimwambia mama yake ,“mimi pia nitaenda, ili aniue kama alivyowaua kaka zangu, au nitamuua.”

Ila mama yake alimwambia: “mwanangu sipendi uondoke. Wale watatu wameshafariki; na wewe kama ukiuawa pia, haitakuwa kidonda kimoja baada ya kingine katika moyo wangu?”

“Vyovyote vile,” alisema, “Siwezi kuacha kwenda; ila usimwambie baba.”

Mama yake alimuandalia keki , na akampa watumishi wa kuondoka naye; alichukua mkuki mzuri, ambao ni mkali kama wembe, na upanga, alimuaga mama yake, na akaondoka.

Kutokana na kuachwa  nyumbani mara nyingi, alishindwa kujua mahali alipokuwa anaenda kuwinda; hivyo alienda kuwinda ndani ya kitongoji chao, alipomuona mbwa mkubwa, aliamini kuwa ndiye mnyama aliyekuwa anamtafuta; hivyo akamuua, alimfunga kamba, na kumuburuza mpaka nyumbani, huku akiimba,

Sehemu ya Pili

“Ooh, mama, nimemuua

Noondah, mla watu.”

Mama aliyekuwa ghorofani, alipomsikia, alichungulia dirishani, na kuona alichokuwa amekileta na kusema, “Mwanangu, huyu siyo noondah, mla watu.”

Hivyo aliuacha mzoga nje na kwenda kuongelea suala hilo, na mama yake alimwambia, “Mwanangu mpendwa, noondah ni mnyama mkubwa kuliko huyo uliyemleta; lakini ningekuwa wewe, ningeiacha hii kazi, na nikakaa nyumbani.”

“Hapana, hakika,” alisema kwa sauti; “sitakaa nyumbani mpaka nikutane na kupigana na noondah.”

Aliondoka tena, na safari hii alienda mbali zaidi ya pale alipofika mwanzo. Mara alimuona paka, na akaamini kuwa yule paka ni mnyama aliyekuwa anamtafuta, alimuua, akamfunga, na kumuburuza mpaka nyumbani, akiimba,

“Ooh, mama, nimemuua

Noondah, mla watu.”

Mama alipomuona yule paka alisema, “Mwanangu, huyu siyo noondah, mla watu.” Akaamua kumtupa.

Mama yake aliendelea kumsihi akae nyumbani, lakini hakumsikiliza, na akaanza kuondoka tena.

Safari hii alienda mpaka msituni, na alipomuona paka mkubwa kuliko yule wa awali, alimuua, alimfunga, na kumuburuza kwenda nyumbani, akiimba,

“Ooh, mama, nimemuua

Noondah, mla watu.”

Lakini mama alipomuona, alimwambia kama mwanzo, “Mwanangu, huyu siyo noondah, mla watu.”

Alijisikia vibaya; na mama yake akamwambia,”Sasa, utampata wapi noondah? Hujui yuko wapi, na haujui anafananaje. Utaumwa, na unaonekana hauna afya njema. Njoo, kaa nyumbani.”

Lakini alimwambia: “Kuna vitu vitatu, na nitafanya kimojawapo: Nitakufa; Nitamtafuta noondah nakumuua; au nitarudi nyumbani bila mafanikio. Katika hali yoyote, ninaondoka.”

Safari hii alienda mbali zaidi ya mwanzo, alimuona pundamilia, akamuua, na kumuburuza mpaka nyumbani, akiimba,

“Ooh, mama, nimemuua

Noondah, mla watu.”

Mama yake alilazimika kumwambia kwa mara nyingine tena, “Mwanangu, huyu siyo noondah, mla watu.”

Baada ya majadiliano, ambapo mama yake alijaribu kumshawishi bila mafanikio, aliondoka tena, kwenda mbali zaidi, alipomkamata na kumuua twiga alisema: “Jambo jema, safari hii nimefanikiwa. Huyu lazima atakuwa noondah.” Hivyo alimuburuza mpaka nyumbani, akiimba,

“Ooh, mama, nimemuua

Noondah, mla watu.”

Kwa mara nyingine mama yake alimjulisha, “Mwanangu, huyu siyo noondah, mla watu.” Kisha akamwambia akae nyumbani kama kaka zake ambao hawahangaiki kumuwinda noondah, na wamekaa na nakuendelea kufanya shughuli zao nyumbani. Lakini alidai kuwa yeye hakuwa sawa na kaka zake, akaonesha msimamo wa kuendelea na kazi yake mpaka apate mafanikio, aliondoka tena, na akaenda umbali mrefu zaidi kuliko awali.

Walipokuwa wakipita nyikani walimuona faru akiwa amelala chini ya mti, akawageukia watumishi wake akawaambia kwa sauti, “Hatimaye nimemuona noondah.”

“Wapi, mkuu?” walipiga yowe, kwa shauku.

“Pale, chini ya mti.”

“Ooh! Tufanye nini?” waliuliza.

Aliwajibu: “Awali ya yote, tule vyakula vyetu, halafu tumvamie. Tumemkuta sehemu nzuri, ingawa kama akituua, tutakuwa hatuna cha kufanya.”

Hivyo wote walichukua keki zao za wanga wakala mpaka wakashiba.

Baadae Mkaa Jikoni aliwaambia, “Kila mmoja wenu achukue bunduki mbili; moja aiweke karibu yake, na nyingine aishike mikononi, na ukifika mda tutafyatua risasi kwa pamoja.”

Na wote wakasema, “Sawa, mkuu.”

Walipita katika vichaka wakitembea kwa umakini, wakatokea upande wa pili wa mti, nyuma ya faru; halafu walisogea karibu yake, na wakamfyatulia risasi kwa pamoja. Yule mnyama aliruka, na kukimbia kwa umbali mdogo, kisha alianguka chini.

Walimfunga, na kumuburuza kwa siku mbili, mpaka walipoufikia mji, na Mkaa Jikoni, alianza kuimba.

Sehemu ya Tatu

“Ooh, mama, nimemuua

Noondah, mla watu.”

Lakini alipata majibu yanayofanana kutoka kwa mama yake: “Mwanangu, huyu siyo noondah, mla watu.”

Watu wengi walikuja na kumuangalia faru, na walimuonea huruma kijana. Mama na baba yake walimsihi aachane na ile kazi ya kumtafuta noondah, baba yake akamuahidi kumpa kitu chochote anachokihitaji endapo ataamua kukaa nyumbani. Lakini alisema, “Sisiskii mnachokisema; kwaherini.” Na aliondoka tena.

Safari hii alienda umbali mrefu zaidi kutoka nyumbani, na hatimaye mida ya saa sita mchana alimuona tembo akiwa amelala msituni. Akawaambia watumishi wake, “Sasa tumempata noondah.”

“Aah, yuko wapi?” waliuliza.

“Pale, kivulini. Mnamuona?”

Walinyemelea kwa uangalifu ndani ya vichaka
Walinyemelea kwa uangalifu ndani ya vichaka

“Ooh, ndiyo, mkuu; tumuendee?”

“Tukimuendea, akiwa anaangalia upande huu, atatuijia, na akituijia, baadhi yetu tutauliwa. Nafikiri itakuwa vizuri mmoja wetu akimkaribia na kuona upande anakoangalia.

Kila mmoja alikubaliana na wazo hilo, kijakazi aliyeiitwa Keerobo′to alitembelea magoti na mikono, na kwenda kumuona. Aliporudi kwa namna ile ile ya kutembelea magoti na mikono, mkuu wake alimuuliza: “Eeenh, taarifa zinasemaje? Ni noondah?”

“Sijui,” alijibu Keeroboto; “Lakini nafikiri bila shaka atakuwa ni yeye. Ni mpana, ana kichwa kikubwa,  mungu wangu, sijawahi ona masikio makubwa kama yale!”

“Sawa,” alisema Mkaa Jikoni; “ngoja tule, halafu tumuendee.”

Kwahiyo walichukua keki zao za wanga, na keki za molasi, wakala mpaka wakashiba.

Baada ya kula, kijana aliwaambia: “Watu wangu, inawezekana leo ikawa siku ya mwisho tutakayoiona; hivyo kila mtu akapate mapumziko. Wale wanaotoroka na watoroke, na wanaokufa na wafe; ila kama nikifa, wale watakaotoroka wawaambie baba na mama yangu wasiomboleze.

Lakini watumishi wake walimwambia , “Ooh, tulia, mkuu; hakuna miongoni mwetu atakayekufa, tumuombe Mungu.”

Walitembelea magoti na mikono mpaka walipomkaribia yule mnyama, wakamwambia Mkaa Jikoni, “ Tuambie cha kufanya, mkuu;” lakini akasema, “Sina mpango wowote, ila tu wote tufyatue risasi kwa pamoja.”

Jambo jema, wote walifyatua risasi kwa pamoja, na mara ghafla tembo aliruka, na kuwakimbiza. Walikimbia kama ndege aina ya helter-skelter! Walitupa bunduki zao, na kila walichobeba, wakakimbilia na kupanda miti kwa spidi kali.

Tembo naye alipokimbia umbali kiasi alidondoka chini.

Wote walibaki mitini kuanzia saa tisa mpaka saa kumi na mbili kamili asubuhi, bila chakula wala mavazi.

Kijana mdogo akiwa juu ya mti alilia kwa uchungu, akisema, “Sijui maana ya kifo, ila kwangu mimi hii ndo itakuwa maana yake,” Kwa kuwa hakuna aliyeweza kumuona mwenzie, hakujua watumishi wake walipo, na akiwa anatamani kushuka juu ya ule mti, alifikiria, “ Labda noondah yupo chini ya mti, atanila.”

Na kila mtumishi alikuwa na mawazo kama ya kijana, alitamani kushuka mtini, ila aliogopa, akihisi kuwa noondah anamsubilia chini amle.

Keeroboto alimuona tembo wakati anaanguka, lakini aliogopa kushuka mtini, akawa anajisemea, “Ingawa kaanguka chini, labda hajafa.” Muda si mrefu alimuona mbwa akimwendea tembo na kumnusa, akapata uhakika kuwa ameshakufa. Alishuka mtini haraka haraka akapiga yowe, na akajibiwa; lakini hakujua upande sauti ilipotokea, alirudia kupiga yowe huku akisiliza kwa makini. Sauti ilipojibiwa aliifata mpaka ilipotokea, na aliwakuta jamaa zake wawili katika mti mmoja.  Aliwaambia, “Jamani, shukeni chini; noondah amekufa.” Walishuka chini haraka na kuanza kumtafuta mkuu wao mpaka wakampata. Walipompa taarifa za kifo cha noondah, alishuka chini pia; baada ya mda mfupi watumishi wote walikuwa wameshakusanyika pamoja na walichukua bunduki na nguo zao, wakawa salama tena. Lakini wote walikuwa wamenyong’onyea wakiwa na njaa, wakapumzika na kula vyakula, baada ya hapo wakaenda kuchukua ushindi wao.

Mara baada ya Mkaa Jikoni kumuona alisema, “Aah, huyu ni noondah! Huyu ndiye! Huyu ndiye!” Na wote walikubaliana kuwa alikuwa ndiye.

Hivyo walimuburuza yule tembo kwa mda wa siku tatu mpaka wakafika mjini, kisha kijana alianza kuimba,

“Ooh, mama, huyu ndiye,

Noondah, mla watu.”

Alikasirika sana mama yake alipomjibu, “Mwanangu huyu siyo noondah, mla watu.” Aliendelea kusema: “Maskini kijana! Umepatwa na nini. Watu wote wanashangaa kuona kijana mdogo kama wewe, unategemewa kuwa na uelewa mkubwa zaidi ya kiasi hiki!”

Baba na mama walianza kumsihi tena, na mwishowe wakakubaliana kuwa safari hii ingekuwa safari yake ya mwisho, bila kujalisha matokeo yoyote atakayoyapata.

Walipiga kambi usiku ule
Walipiga kambi usiku ule

Jambo jema, walianza safari tena, walitembea na kutembea, wakaupita msitu, hadi walipoufikia mlima mrefu, wakaamua kuweka kambi na kulala chini ya mlima.

Sehemu ya Nne

Kulipokucha asubuhi walipika na kula wali, halafu Mkaa Jikoni akasema: “Sasa tupande mlima, na tuiangalie nchi yote tukiwa kileleni.” Walikwenda, walikwenda, na baada ya mda mrefu, wakiwa wameshachoka, walifika kileleni, wakapumzika wakiwa wanapanga mipango yao.

Mmoja wa watumishi aitwaye Shindaa′no, wakati akiwa anatembeatembea, aliangalia chini ya mlima, na mara alimuona mnyama mkubwa kwa mbali; lakini kutokana na umbali na miti mingi, hakuweza kumuona vizuri. Alimuita mkuu wake, akamuonesha, na kuna kitu ndani ya moyo wa Mkaa Jikoni kilimwambia kuwa yule alikuwa noondah. Ili kujiridhisha, alichukua bunduki na mkuki wake, alishuka mlimani ili aweze kumuona vizuri.

“Aah,” alisema, “huyu lazima atakuwa noondah. Mama yangu aliniambia masikio yake ni madogo, na yale ni madogo; aliniambia kuwa noondah ni mpana na mfupi, na huyu ndivyo alivyo; alisema ana madoa mawili kama paka, madoa yale pale; aliniambia mkia wake ni mnene, na mkia mnene ule pale. Lazima atakuwa noondah.”

Aliwaendea watumishi wake na kuwamuru wale chakula, na wakafanya hivyo. Kisha aliwaambia waache vitu vyote visivyokuwa na umuhimu, kwasababu kama wakitakiwa kukimbia waweze  kukimbia vizuri bila vizuizi, na kama wakishinda pambano watarudi kuchukua mizigo yao.

Baada ya kuiweka sawa mipango yao walianza kuteremka mlima, lakini walipokuwa wametembea nusu ya umbali  Keeroboto na Shindaano waliingiwa na hofu. Kisha kijana aliwatia moyo wenzake: “Ooh, twende; msiogope. Sisi sote tunaishi na kufa. Mnaogopa nini?” Baada ya kuwatia moyo waliendelea na safari.

Walipokaribia eneo lile, Mkaa Jikoni aliwaamuru kuvua nguo zao isipokuwa wabaki na nguo moja inayowabana sana ili kama ikitokea wakakimbia wasinase kwenye miiba na kwenye matawi ya miti.

Walipomsogelea yule mnyama, walimkuta amelala, na wote wakakubaliana kuwa alikuwa noondah.

Kisha kijana akasema, “Sasa jua linazama, tumpige risasi, au tusubilie mpaka asubuhi?”

Na wote walitamani kufyatua risasi mara moja, ili waweze kuona matokeo yatakuwaje pasipo kuendelea kuwa na sintofahamu. Kwahiyo wote walipanga kufyatua risasi kwa pamoja.

Wote walisogea karibu, na mkuu alipotoa neno, wote walifyatua  risasi kwa pamoja. Noondah hakuweza hata kusogea; pigo moja lilimtosha. Hata hivyo wote walitawanyika na kukimbilia juu mlimani. Usiku ule walikula na kupumzika.

Ilipofika asubuhi walikula wali wao, kisha waliteremka mlimani na kwenda kuona kilichotokea, wakamkuta yule mnyama akiwa ameshakufa.

Baada ya kula na kupumzika, walianza safari ya kurudi nyumbani, wakiwa wanauburuza ule mzoga wa mnyama. Ilipofika siku ya nne wakiwa njiani yule mnyama alianza kuonesha dalili za kuoza, na watumishi wakatamani wamuache njiani; lakini Mkaa Jikoni aliwaambia waendelee kumuburuza hata kama atabakia mfupa mmoja.

Walipoukaribia mji alianza kuimba,

“Mama, mama, nimekuja

Kutoka kwenye mizimu, nyumbani.

Mama, nisikilize nikiimba;

Nikiwa nakwambia nilicholeta.

“Ooh, mama, nimemuua

Noondah, mla watu.”

Na mama alipomwangalia, alilia, “Mwanangu, huyu ni noondah, mla watu.”

Kisha watu wote walikuja kumkaribisha, na baba yake alijawa na furaha, alimpa heshima, na alimtafutia mwanamke mzuri na tajiri; Baada ya baba yake kufariki Mkaa Jikoni akawa sultani, na aliishi miaka mingi akiwa mweye furaha, na alipendwa na watu wote.

Kwa nakala zaidi zinazohusu hadithi bofya hapa!