Uongozi wa Mwinyi na Mageuzi ya Sera za Ujamaa za Nyerere
Orodha ya Yaliyomo
Rais Julius Nyerere alistaafu mnamo Oktoba 1985 na kumchagua Ali Hassan Mwinyi kuwa mrithi wake. Nyerere alibakia kuwa mwenyekiti wa chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM), hadi 1990, hali ambayo baadaye ilisababisha mvutano kati ya serikali na chama kuhusu itikadi ya mageuzi ya uchumi. Wakati wa ubadilishaji wa madaraka upokuwa ukifanyika, uchumi wa Tanzania ulikuwa katikati ya kuporomoka. Kuanzia 1974 hadi 1984, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 2.6 kwa mwaka wakati idadi ya watu iliongezeka kwa kasi ya 3.4% kila mwaka. Mapato ya vijijini na mishahara ya mijini vyote vilikuwa vimeshaanguka tayari kwenye miaka ya 1980, licha ya sheria za kima cha chini za mishahara kuwepo. Zaidi ya hayo, sarafu ya Tanzania ilikuwa na thamani zaidi, kitu kilichofanya bidhaa za msingi kuwa chache, na
nchi ilikuwa na zaidi ya dola bilioni tatu za deni la nje. Uzalishaji wa kilimo ulikuwa chini, na maoni ya ujumla kwa wakati huo yalikuwa ni kwamba sera za Ujamaa za Nyerere zimeshindwa kiuchumi.
Sera kama hizo zilijumuisha utaifishaji wa mashirika yalikuwa yanafanya uzalishaji mkubwa, uhamishaji wa kulazimishwa watu vijijini kwenda kuishi katika mashamba ya umoja, na upigaji marufuku wa vyama vya upinzaji. Wafuasi wa Nyerere walipinga kuhusisha Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia katika mageuzi ya uchumi wa ndani, kwa sababu waliamini vyombo hivi vingesababisha kukosekana kwa utulivu na kuleta mgongano na maadili yao ya ujamaa. Pia, uhusiano wa Tanzania na IMF ulikuwa umeharibika tayari kwani serikali ya Nyerere ilishindwa kutimiza masharti ya mkopo uliotolewa kwa makubaliano ya kifurushi cha kifedha cha 1980.
Mwanzoni mwa mabadiliko haya ya kisiasa, watu wengi waliamini kwamba Mwinyi hasingeweza kupingana au kuacha sera za Nyerere kwani alikuwa mfuasi mwaminifu wa mtangulizi wake. Walakini, Ali Hassan Mwinyi na wafuasi wake walitaka mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ili kukomboa soko na kuhoji upya itikadi za jadi za ujamaa. Mwinyi alihakikisha amezungukwa na wanaharakati wa mageuzi, kiasi cha kubadilisha nafasi ya washiriki watatu wa baraza la mawaziri na mawaziri wengine ambao walipinga mabadiliko. Waziri Mkuu wakati huo, Joseph Warioba, pamoja na waziri wa fedha Clement Msuya pia walikuwa wanaunga mkono sera mpya. Wakati wa hotuba yake ya kwanza kwa Bunge la Tanzania mnamo 1986, aliahidi kuanza mazungumzo na IMF na Benki ya Dunia, akizingatia kwamba makubaliano yoyote yanayotokana na mazungumzo hayo yatakuwa na faida kwa raia wa Tanzania.
Mikataba na Taasisi za Fedha za Kimataifa
Mnamo mwaka wa 1986, Mwinyi alifanya makubaliano na IMF kupata mkopo wa kusubiri (kwa kiingereza ni standby loan) wa dola milioni 78, ambao ulikuwa ni mkopo wa kwanza wa nje wa Tanzania wa zaidi ya miaka sita. Baadaye, wadhamini wa mkopo huu waliidhinisha
mpango kubadili tena muda wa malipo ya deni. Walikubali kufanya hivyo kwa kipindi cha miaka mitano, lakini walihitaji Tanzania kulipa tu 2% ya deni lao kwa wakati huo. Katika mahojiano, Mwinyi alizitaka nchi za wafadhili kutumia Canada kama mfano na kufuta madeni yote ya Tanzania kwa pamoja. Na kama ombi hilo halikuwezekana, basi aliomba deni lilipwe ndani ya miaka kumi, ingawa miaka ishirini au ishirini na tano ilikuwa ndio muafaka zaidi. Alitabiri kwamba ifikapo wakati huo, uchumi wa nchi utakuwa mzuri na katika hali bora ya kulipa deni bila kuumiza nchi. Katika mahojiano hayo hayo, Mwinyi aliomba wafadhili watoe mikopo yenye viwango vya chini vya riba.
Mwinyi alidai kuwa mazungumzo yake na IMF yalikuwa ni kwa niaba ya watu: kwa mfano, alikubali ombi la Mfuko kwamba apunguze idadi ya taasisi za umma, lakini katika wakati ambao jambo hilo lilikuwa ni lazima na kama linawezekana kufanywa hatua kwa hatua. Isitoshe, alikataa pendekezo lao la kusimamisha kuongezeka kwa mishahara ndani ya serikali na kupunguza huduma za umma za bure.
Mwaka uliofuata, Mwinyi alijadili kituo cha kwanza cha marekebisho ya muundo (SAF) na IMF, kilichofuatiwa na makubaliano mengine baadaye mnamo mwaka 1988 na tena mnamo mwaka 1990. Mbali na maendeleo haya, Benki ya Dunia ilitoa mikopo ya muundo wa marekebisho katika kilimo, viwandani, sekta za kifedha. mnamo 1989, Rais Mwinyi alianza awamu ya pili ya mpango wake wa marekebisho kwa kusudi la kurekebisha sekta za kijamii, haswa kwa kuongeza matumizi ya serikali kwenye elimu.
Siasa za vyama vingi
Mnamo 1991, hatua za kwanza za mpito kuelekea kwenye vyama vingi zilianza wakati Mwinyi alipomteua Jaji Mkuu Francis Nyalali kuongoza tume ya kuchunguza kiasi cha umaarufu wa mfumo wa chama kimoja. Tume hii iliwasilisha ripoti yao kwa Rais mnamo 1992, ikipendekeza kwamba serikali ibadilishe na nchi iwe na mfumo wa vyama vingi. Walitoa pendekezo hili licha ya ukweli kwamba ni asilimia ishirini na moja tu kati ya watanzania 36,299 walihojiwa walikubali mabadiliko haya. Walakini, asilimia hamsini na tano ya asilimia sabini na saba waliounga mkono mfumo uliokuwepo walikuwa wanapendelea mageuzi ya aina fulani. Jaji Nyalali aliorodhesha sheria maalum ishirini ambazo zilihitaji kurekebishwa ili kuzingatia mahitaji ya mfumo wa vyama vingi. Mwinyi aliunga mkono pendekezo lao na Mkutano wa Kitaifa wa CCM uliridhia mabadiliko na kupitia marekebisho ya katiba mnamo Februari 1992. Walakini, sio sheria zote ishirini zilizrekebishwa, pamoja na Sheria ya Uzuiaji wa kumweka Rais kizuizini iliyoachwa kutoka nyakati za ukoloni.
Rushwa
Wakati wa miaka ya urais wa Julius Nyerere, ufisadi ulionekana kama aina ya kukandamiza ambayo inadhoofisha maadili ya usawa ya Tanzania. Lakini, ripoti za ufisadi ziliongezeka pamoja na nguvu ya uchumi ilivyozidi kukuwa. Chini ya urais wa Mwinyi, tabia za rushwa zilizidi kuwa mbaya na nyingi licha ya sera zake za ukombozi wa kiuchumi. Hali ilikuwa mbaya hadi wafadhili wengine wakahamuwa kusimamisha misaada mnamo 1994 kama jawabu la tatizo hilo. Wakati wa uchaguzi wa vyama vingi vingi mnamo 1995, vyama vya upinzani vilitumia hasira za watu juu ya ufisadi uliondelea kama mafuta ya kisiasa. Walakini, mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa aliweza kutumia manung’uniko hayo ya rushwa kama silaha yake, kwani alionekana kuwa mtu ambaye hajachafuliwa na rushwa au kashfa zozote za ufisadi zilizoambatana na utawala wa Mwinyi.
1993 Kashfa ya Chavda
Ndugu na wafanyabiashara wanaojulikana kama V.G. Chavda na P.G. Chavda walipokea mkopo wa $ milioni 3.5 kutoka kwa mpango wa ubadilishaji wa deni (DCP) mnamo 1993. Waliahidi kutumia pesa hizi kurekebisha mashamba yaliyokuwa yanakufa jijini Tanga. Hii ni pamoja na kuboresha makazi ya wafanyakazi, kukarabati mashine za zamani, na kulima mashamba upya. Walidai miradi yao italeta ajira 1,400 na itatoa dola milioni 42 kwa pesa za fedha za kigeni. Lakini kilichotokea, walikuwa wameelekeza fedha nje ya nchi kupitia ununuzi wa mashine bandia na vifaa. Baadaye pia iligundulika kwamba wanasiasa wa hali ya juu walikuwa wanawasaidia, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nyumbani, Augustine Mrema. Waliweza kukwepa mashtaka.
Mohamed Enterprise
Mwanzoni mwa 1995, kampuni inayojulikana Mohamed Enterprise ilishtumiwa kwa madai ya kusambaza chakula ambacho hakifai kwa matumizi. Mrema alidai angeiadhibu kampuni hiyo, lakini alibatilishwa cheo chake kuwa Waziri wa Vijana na Utamaduni kabla ya kuchukua hatua. Alikosoa utawala wa Mwinyi kwa kuvumilia viwango vya juu vya ufisadi na kutojishughulisha kikamilifu juu ya utekelezaji wa vita dhidi ya rushwa. Kilichofuata ni Mrema kuondolewa katika baraza la mawaziri, na ndipo baada ya hapo akawa mgombea katika moja ya vyama vya upinzaji, NCCR-Mageuzi.
Maoni juu ya ubaguzi wa rangi
Katika mahojiano ya 1988 alipoulizwa juu ya maoni yake kuhusu ubaguzi, Mwinyi alisema kwamba vikwazo vikali, kamili vilihitajika kutekelezwa dhidi ya Afrika Kusini. Alitaka pia mataifa ya Magharibi kusaidia “mataifa ya mstari wa mbele” katika kushughulikia majaribio yoyote ya uharibifu yaliyokuwa yakifanywa na serikali ya Afrika Kusini dhidi ya wale waliokuwa wanaipinga. Mwinyi alisema kufanya mambo haya kungemaliza Ubaguzi. Alitaja kusitasita kwa utawala wa Reagan katika kutekeleza vikwazo vikali kuwa “changamoto kubwa” na akaelezea matumaini yake kuwa viongozi wa baadaye wa Amerika watachukua hatua zaidi dhidi ya serikali ya Afrika Kusini.
Kuna mengi mno ya kujuwa kuhusu uongozi wa Mwinyi na mabadiliko ya kisiasa na uchumi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama unapenda kupata makala zaidi zinazohusu mada zinazoshabihiana, gonga hapa!